Mazungumzo na "Kingunge" wa Itikadi ya Ujamaa

(0 User reviews)   2028   1575
By OLS Admin Posted on Mar 23, 2021
In Category - Kutoka Kavazini
Prof. Issa Shivji 978-9976-5483-0-3 Kavazi la Mwalimu Nyerere 2019
Kitabu hiki kimebeba mazungumzo aliyofanya Profesa Issa Shivji na hayati Mzee Ngombale kwa wakati na madhumuni tofauti. Kutokana na umuhimu wake wa kipekee, Kavazi la Mwalimu Nyerere limeona ni sehemu ya jukumu lake kuchapisha na kuiwekea rekodi ya kudumu ya mchango wa mwanasiasa na mwanazuoni wetu mahiri, Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru.

Kitabu hiki kimebeba mazungumzo niliyofanya na marehemu Mzee Ngombale kwa nyakati na madhumuni tofauti. Tarehe 27 Agosti 2009 nilizungumza naye kwa lengo la kuyachapisha mazungumzo hayo katika Jarida la Chemchemi, ambalo lilikuwa linachapishwa na Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mazungumzo ya pili nilifanya naye kwa tarehe tofauti miaka mitatu baadae (19/06/2012, 7/08/2012, 10/08/2012 na 16/08/2012) kwa ajili ya kitabu cha wasifu wa Mwalimu Nyerere ambacho tunaandika wanazuoni watatu (Issa Shivji, Saida Yahya-Othman na Ng’wanza Kamata). Mazungumzo haya yamehaririwa na Saida Yahya-Othman na yanachapishwa kwa mara ya kwanza katika kitabu hiki.

Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru ni kiongozi anayejulikana sana na Watanzania. Yeye ana nafasi ya kipekee katika historia ya kisiasa nchini kwa sababu ametumika, katika nyadhifa mbalimbali za Chama-tawala na Serikali, awamu zote nne za utawala. Umahiri wake unajulikana hasa katika medani ya itikadi na falsafa ya U-Marx juu ya usoshalisti wa kisayansi. Mzee Ngombale alikuwa mstari wa mbele katika kuandika rasimu za nyaraka muhimu sana na za kihistoria za Chama pamoja na Mwongozo wa TANU wa mwaka 1971 na Mwongozo wa CCM wa mwaka 1981. Chanzo na sababu za Chama kuandaa Miongozo hii miwili imeelezwa kwa ufasaha na Mzee Ngombale na kwa maoni yetu ni kumbukumbu muhimu ya kihistoria ambayo haina budi kuwekwa kwenye rekodi ya kudumu kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Pamoja na umahiri wake wa kuchambua kwa undani masuala ya kiitikadi, Mzee Ngombale pia alikuwa anajulikana kwa msimamo wake thabiti. Ndiyo maana wengi wetu tulishtuka kidogo alipochukua msimamo wa kuunga mkono mgombea wa upinzani katika uchaguzi wa 2015. Kama kawaida yake alielezea hadharani sababu zake za kufanya hivyo, sababu mojawapo ni kwamba Chama chake kilikiuka tarataibu za Chama chenyewe za kupendekeza mgombea wa urais. Inawezekana wengi wa mashabiki wake wasikubaliane na mantiki ya sababu alizotoa lakini pamoja na kutokubaliana naye, kwa maoni yangu, wachache sana wanaweza kuzipuuza sababu alizotoa.

There are no reviews for this eBook.

0
0 out of 5 (0 User reviews )

Add a Review

Your Rating *

Related eBooks