Azimio la Arusha: Majibu kwa Maswali

(0 User reviews)   2369   1381
By OLS Admin Posted on Mar 23, 2021
In Category - Occasional Papers
Julius K. Nyerere 978-9976-9903-7-9 Kavazi la Mwalimu Nyerere 2017
Katika kuitikia tangazo la Azimio la Arusha, wabunge waliwasilisha takriban maswali 21 kuhusiana na Azimio hilo ambayo yalijibiwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe kama ilivyo katika kijitabu hiki. Madhumuni ya kuchapisha kijitabu hiki ni kuwakumbusha vijana wetu historia ya Azimio na kuibua mjadala kuhusu mazingira ya leo na somo gani tunaweza kujifunza.

Miezi miwili tu baada ya kupitishwa kwa Azimio la Arusha katika kikao cha Halmashauri ya Chama, TANU, mwishoni mwa Januari 1967, Mzee Kawawa aliwatangazia wabunge kwamba kama wana maswali juu ya Azimio wayawasilishe na yatajibiwa. Katika kuitikia wito huo wabunge waliwasilisha takriban maswali 21 ambayo yalijibiwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe. Kama tujuavyo, Azimio la Arusha lilikuwa na mambo mawili makubwa (angalia chapisho la Kavazi liitwalo Simulizi za Azimio la Arusha, 2017). Mosi, ni utaifishaji wa njia kuu na nyeti za uchumi na, pili, utungwaji wa miiko ya viongozi wa serikali, mashirika ya umma na chama. Utaifishaji uliwagusa moja kwa moja mabepari wa nje ambao walikuwa wanamiliki viwanda, mabenki, bima, migodi ya madini na biashara ya jumla ya nje.

Walikuwemo pia mabepari wa ndani ambao wakati ule wengi walikuwa Watanzania wenye asili ya kihindi. Hao walikuwa wanamiliki viwanda vichache lakini zaidi vinu vya kusindika na kusaga nafaka. Utaifishaji haukuwapendeza mabepari wa nje na nchi zao ingawa wasingeweza kuupinga kwa sababu serikali aliwaahidi fidia. Kwa hivyo, mvutano ukawa kuhusu kiwango cha fidia na masharti ya ulipaji wake.

Ndani ya nchi, viongozi na wananchi walifurahia sera ya utaifishaji na waliipokea kwa mikono miwili. Lakini viongozi, sio wananchi, hawakupenda kabisa miiko ya uongozi, hususan, kile kifungu kilichowazuia kumiliki nyumba za kukodisha. Viongozi wengi, mara baada ya uhuru, walianza kujenga nyumba za kukodisha ili kujiongezea mapato. Hata katika kikao cha Halmashauri miiko ndiyo iliyowapa viongozi wengi shida, wakiwemo wanachama mashuhuri kama Mzee Rupia. Malalamiko dhidi ya miiko ya uongozi yaliendelea kichinichini na yanajitokeza waziwazi katika maswali yaliyowasilishwa na wabunge. Takriban maswali yote yalikuwa juu ya masharti ya uongozi na hakuna hata moja lililohusu ujamaa.

Madhumuni yetu ya kuchapisha kijitabu hiki ni, mosi, kuwakumbusha vijana wetu historia ya Azimio katika mwaka huu wa 50 tangu kuzaliwa kwake na pili, kuibua mjadala kuhusu mazingira ya leo na somo gani tunaweza kujifunza kutokana na Azimio la Arusha.

There are no reviews for this eBook.

0
0 out of 5 (0 User reviews )

Add a Review

Your Rating *

Related eBooks