Uanazuoni wa Mwalimu Nyerere
Karibu asilimia 85 ya Watanzania wa leo hawakupata nafasi ya kumuona Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mbali na hotuba zake chache zinazosikika mara kwa mara kwenye vyombo vya habari, ni wachache sana ambao wamepata nafasi ya kusoma maandishi yake kwa undani. Hivyo basi, wengi wa vijana wetu leo hii, hawajapata nafasi ya kumuelewa vizuri Mwalimu Nyerere na falsafa yake ya uongozi na mambo ya msingi aliyoyasimamia kama Baba wa Taifa letu.
Wanazuoni wa Kitanzania wakiongozwa na Prof. Issa Shivji wanawasilisha sehemu ya matokeo ya mradi wa utafiti juu ya fikra za kisiasa za Baba wa Taifa unaogharimiwa na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia. Lengo kuu la mradi huu ni kuandika kitabu juu ya maisha ya Baba wa Taifa. Baada ya uandishi kukamilika, kitabu hicho kitakuwa ni cha kwanza cha kina kuandikwa na Watanzania. Hadi leo vitabu vyote vilivyoandikwa juu ya maisha ya Mwalimu ni vya wageni.
Katika kitabu hiki, waandishi wanamuelezea Baba wa Taifa kama mwanafalsafa, mwanazuoni, mshairi na pia mmajumui wa Kiafrika. Ninashukuru na kufurahi kupata fursa ya kuandika utangulizi wa kitabu hiki kama sehemu ya mwanzo ya kuwasilisha matokeo ya utafiti juu ya maisha ya Baba wa Taifa kwa Watanzania na wasomaji wengine wa Kiswahili. Matokeo ya utafiti huu yanatoa nafasi kwa makundi mbalimbali ya jamii yetu kumuelewa Mwalimu kwa njia rahisi na nzuri zaidi; miongoni mwa makundi hayo ni wanasiasa na viongozi wanaochipukia hivi sasa na vijana wenye kutaka maendeleo ya kweli ya Taifa letu. Ni fursa nzuri pia kwa watafiti na wanazuoni kuelewa misingi ya misimamo ya Mwalimu ambayo inaweza kuwa ni nyenzo nzuri ya kufanya utafiti, machocheo, uchambuzi na udadisi anuai. Kwa Watanzania wachache ambao walikuwepo wakati wa uongozi wa Mwalimu hii ni nafasi nzuri kwao ya kujikumbusha na kutafakari baadhi ya mambo yaliyotokea wakati huo na misingi ya misimamo yake.